You are currently viewing ZFDA YATOA ELIMU KWA WADAU WA MADUKA YA DAWA ZA WANYAMA

ZFDA YATOA ELIMU KWA WADAU WA MADUKA YA DAWA ZA WANYAMA

  • Post author:
  • Post category:Public / ZFDA

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) imeendesha mafunzo kwa wadau wa maduka ya dawa za wanyama kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo na namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika matumizi ya dawa hizo.

Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa ZFDA, Mombasa, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkaguzi Mkuu wa Dawa wa ZFDA, Abdulfatah Nassor Issa, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kutoa ushauri kwa wadau, kusikiliza changamoto zao pamoja na kuwapatia elimu kuhusu matumizi sahihi na salama ya dawa za mifugo.

Amesema matarajio ya ZFDA ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili wadau hao zinapatiwa ufumbuzi, huku usalama dawa ukiendelea kuimarishwa na kufikia viwango vya hali ya juu, jambo litakalosaidia kulinda afya za wanyama na watumiaji wa bidhaa zinazotokana na mifugo.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa ZFDA, Fatuma Makame Juma, amewataka wadau hao kuhakikisha wanatoa maelekezo sahihi kwa wafugaji kuhusu matumizi ya dawa za mifugo, akieleza kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wafugaji kutumia dawa kiholela na kuchinja wanyama bila kufuata utaratibu unaotolewa na wataalamu.

Amesema matumizi yasiyo sahihi ya dawa yanaweza kuleta madhara kwa wanyama pamoja na afya za binadamu wanaotumia bidhaa zitokanazo na mifugo hiyo.

Kwa upande wao, wadau walioshiriki mafunzo hayo wamepongeza ZFDA kwa hatua hiyo, wakisema elimu waliyoipata wataitumia katika kazi zao na kuwafikishia wafugaji maarifa sahihi kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo, huku wakitoa mapendekezo ya kuendelea kufanyika kwa mafunzo kama hayo mara kwa mara.