You are currently viewing ZFDA Yateketeza Tani 3 za Dawa na Vipodozi Visivyofaa kwa Matumizi ya Binadamu

ZFDA Yateketeza Tani 3 za Dawa na Vipodozi Visivyofaa kwa Matumizi ya Binadamu

  • Post author:
  • Post category:Public / ZFDA

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) unaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha usalama wa afya ya jamii kwa kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba vinavyotumika nchini.

Akizungumza wakati wa zoezi la uteketezaji wa dawa na vipodozi visivyofaa kwa matumizi ya binadamu, Afisa Uhusiano wa ZFDA, Ndg. Fatuma Makame Juma, amesema uteketezaji wa bidhaa hizo ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Wakala pale bidhaa zinapobainika kutokuwa salama au kutokidhi matakwa ya kisheria.

Zoezi hilo limefanyika leo, tarehe 15 Agosti 2026, katika mtambo maalum wa kuchomea taka (Incinerator) uliopo Kibele, Zanzibar, ambapo jumla ya tani tatu (3) za bidhaa zimeteketezwa, zikiwemo tani mbili (2) za vipodozi na tani moja (1) ya dawa.

Ndg. Fatuma amesema miongoni mwa vipodozi vilivyoteketezwa ni vile vyenye viambata sumu ( Mercury, Hydroquinone, Steroids) ambavyo matumizi yake yasipodhibitiwa, yanaweza kusababisha madhara mbalimbali kwa afya ya binadamu.

Ameeleza kuwa matumizi ya vipodozi vyenye viambata hivyo yanaweza kusababisha kuharibika na kuwashwa kwa ngozi, kuungua kwa ngozi, kubadilika kwa rangi ya ngozi, ngozi kuwa nyembamba na dhaifu, pamoja na kupunguza uwezo wa ngozi kujikinga dhidi ya mionzi ya jua. Aidha, baadhi ya viambata hivyo vinaweza kufyonzwa na mwili na kuathiri viungo vya ndani kama figo na ini, na kwa baadhi ya kemikali, madhara yanaweza pia kuhusisha mfumo wa uzazi.

Aidha, Afisa Uhusiano huyo ameeleza kuwa tatizo la vipodozi vyenye viambata sumu halihusu afya ya binadamu pekee, bali pia linaweza kuwa na athari kwa mazingira endapo bidhaa hizo zitatupwa kiholela. Viambata hatarishi vinaweza kuingia kwenye udongo na vyanzo vya maji na hivyo kuathiri mazingira pamoja na viumbe hai.
Amesema kuwepo kwa mtambo maalum wa Incinerator uliopo Kibele kunarahisisha zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo kwa njia inayodhibitiwa, badala ya bidhaa hatarishi kutupwa ovyo na kusababisha uchafuzi wa mazingira.

ZFDA imeendelea kuwataka wafanyabiashara, waagizaji na wasambazaji kuacha kuingiza, kusambaza au kuuza dawa na vipodozi ambavyo havikidhi matakwa ya usalama na ubora, hususan vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku. Wananchi nao wamehimizwa kuwa waangalifu wakati wa kununua vipodozi na kuzingatia taarifa za viambata vilivyomo katika bidhaa husika.

Ndg. Fatuma amesisitiza kuwa mfanyabiashara atakayebainika kukiuka matakwa ya sheria na kanuni zinazosimamiwa na ZFDA atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.