A. Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) umepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuhusu uwepo wa dawa ambazo zimeonekana kuwa na viambata chafuzi (contaminants) katika kiwango kisichoruhusiwa na kinachoweza kusababisha madhara ya kiafya ikiwa ni pamoja na vifo kwa watumiaji, hususani watoto.
Dawa hizo ni;
a. Promethazine Oral Solution,
b. Kofexmalin Baby Cough Syrup,
c. Makoff Baby Cough Syrup na
d. Magrip N Cold Syrup.
B. Dawa zote hizi zinatengenezwa na kiwanda cha Maiden Pharmaceuticals Limited (Haryana India). Dawa hizi zimepatikana nchini Gambia na WHO wanahofia kuwa huenda dawa hizi zikasambazwa na kuenea katika nchi nyingine kwa njia zisizo rasmi. Kwa mujibu wa WHO, Uchunguzi wa kimaabara uliofanywa kwa dawa hizi, umethibitisha kuwa dawa zote hizo zina kiwango kikubwa cha viambata chafuzi (contaminants), diethylene glycol na ethylene glycol, zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa katika dawa za binadamu.
C. ZFDA inapenda kuuhakikishia umma wa wazanzibari kwamba dawa hizi zote hazipo kwenye soko letu na wala hazijawahi kusajiliwa kwa lengo la kutumika hapa Zanzibar. Baada tu ya kupata taarifa hii, ZFDA kwa kutumia mifumo yake, ilichukua hatua za kiudhibiti ili kubaini uwepo wa dawa hizo na kuhakikisha kuwa dawa hizo haziingii Zanzibar
D. Pamoja na hivo, ZFDA inatoa wito kwa Wazanzibari wote kutoa taarifa Ofisi za ZFDA Unguja na Pemba, Ofisi za Waganga/Wafamasia wa Wilaya au Vituo vya Polisi endapo watabaini kuwepo kwa dawa hizo mahali popote ili hatua za haraka za kiudhibiti zichuchukuliwe.