You are currently viewing TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

  • Post author:
  • Post category:ZFDA

KUHUSU JUISI YA APPLE AINA YA CERES YENYE SUMUKUVU PATULIN

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA) ni Taasisi ya Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ambayo pamoja na kazi nyengine ina jukumu la kusimamia Usalama wa vyakula vinavyozalishwa na kuingia Zanzibar kwa mujibu wa Sheria ya Chakula Dawa na Vipodozi Nambari 2/2006 na marekebisho yake.

Mnamo tarehe 11 Oktoba 2021, Kamisheni ya Ushindani ya COMESA (Common Market for Eastern and Southern Africa Competition Commision) ilitoa taarifa ya uwepo wa juisi ya Apple aina ya Ceres ambayo imebainika kuwa na sumukuvu aina ya Patulin katika matoleo ya tarehe 14 hadi 30 Juni, 2021.

Patulin ni sumu inayozalishwa na kuvu aina ya Aspergillus, Byssochlmys na Penicillium ambao huanza kuota ikiwa matunda ya Apple yameanza kuoza. Madhara yanayoweza kupatikana kwa kula matunda yaliyoathiriwa na sumukuvu hiyo ni pamoja na kuchafuka tumbo, kichefuchefu na kutapika. Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Nchi ambazo zimebainika kuwepo na bidhaa hizo mpaka sasa ni pamoja na  DRC (Congo), Seychelles, Zambia na Zimbabwe.

ZFDA ilifanya ukaguzi wa haraka ili kufuatilia kama kuna uwepo wa bidhaa hiyo sokoni kwa:

  1. Kuchambua tena maombi ya uingizaji wa bidhaa yaliyowasilishwa tokea mwezi Juni, 2021 ili kuona kama kuna shehena ya juisi hiyo ipo njiani kuja Zanzibar.
  2. Kufanya Ukaguzi wa Majengo ya uuzwaji wa Vyakula ikiwemo Ghala za kuhifadhia chakula, maduka ya jumla, rejareja na “Supermarkets” ili kuthibitisha uwepo wa matoleo ya kuanzia Juni 14 hadi 30, 2021.

Baada ya Uchambuzi na Ukaguzi huo ulionyesha kuwa bidhaa ya juisi ya Apple aina ya Ceres yenye matoleo ya tarehe hizo HAYAJAINGIZWA ZANZIBAR.

ZFDA itaendelea na  kazi zake za Ukaguzi  na Udhibiti na kuhakikisha kuwa chakula kinachokuwepo kwenye soko la Zanzibar ni salama kwa matumizi ya binaadamu.

Kwa maelezo Zaidi wasiliana nasi kwa simu nambari (024)2233959/0777139968 au baruapepe: info@zfda.go.tz .

Imetolewa na;

SULEIMAN AKIDA RAMADHAN

Kny: MKURUGENZI

IDARA YA UDHIBITI USALAMA WA CHAKULA

ZFDA

Pakua taarifa hii hapa

Please follow and like us: