You are currently viewing TAARIFA YA KUTOKEA KWA MRIPUKO WA MAFUA YA NDEGE “BIRD FLUE”  NCHINI POLAND NA UKRAINE

TAARIFA YA KUTOKEA KWA MRIPUKO WA MAFUA YA NDEGE “BIRD FLUE” NCHINI POLAND NA UKRAINE

  • Post author:
  • Post category:Public / ZFDA

TAARIFA KWA UMA

Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya inayofanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Na. 2/2006 na marekebisho yake Na.3/2017 yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi.

Katika kufanikisha jukumu la kulinda afya ya jamii, ZFDA inafanya ukaguzi na udhibiti wa ubora na usalama wa Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba katika maeneo ya biashara, uzalishaji, uhifadhi na bandarini. Aidha inafuatilia kwa ukaribu zaidi athari zinazotokana na chakula kisicho salama ikiwemo miripuko ya maradhi mbali mbali ili kuweza kuilinda jamii kutokana na madhara yanayoweza kujitokeza.

Mripuko wa ugonjwa wa mafua ya ndege (Bird Flue) umeripotiwa kujitokeza nchini Poland na Ukraine, hali iliyopelekea baadhi ya nchi kuweka zuio la uingizaji wa bidhaa za nyama ya ndege “poultry meat & poultry products” kutoka nchi hizo.

Katika taarifa iliyoripotiwa na Afisa mkuu wa Mifugo kupitia Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Miji nchini Poland, inataja kuthibitishwa juu ya hali ya mripuko wa mafua ya ndege “birds flu”, iliyotokea mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2019.

Mamlaka ya Poland imethibitisha kutokea kwa miripuko tisa (9) ya “bird flu”,  iliyoripotiwa kwa kipindi hichi ambayo imeathiri zaidi ya mifugo 120,000 kwenye baadhi ya mashamba.

Hata hivyo, Wakala wa Usalama wa Chakula na Kumlinda Mlaji nchini Ukraine, imeripoti World Organisation for Animal Health  mripuko wa ugonjwa huo na imeanza kuchukua hatua za kuzuia mripuko huo kuendelea.

Ugonjwa wa mafua ya ndege ni aina ya mafua yanayoenezwa na virusi (Virus – H5N8) wanaotokea kwenye ndege pori. Lakini pia mafua haya yana uwezo wa kuambukiza ndege wanaofugwa–kuku, bata, kanga, n.k.

Ugonjwa huu unaambukizwa kupitia ndege kwa ndege; na kutoka ndege virusi humshika binadamu kupitia vinyesi, majimaji, damu, nguo, au chochote kilichojigusa na ndege aliyeathirika.

Ugonjwa wa mafua ya ndege huwa na dalili zifuatazo kutegemeana na aina ya virusi waliomshambulia muhusika. Maambukizi yanayosababishwa na virusi vya jamii ya H5N8 kwa binadamu husababisha mgonjwa kuwa na dalili zote za mafua makali kama vile:

  • Kukohoa (kikohozi kikavu au wakati mwingine kinachotoa makohozi)
  • Kichefuchefu, kutapika na kuharisha sana, kupumua kwa shida, (Acute Respiratory Distress Syndrome)
  • Homa zaidi ya nyuzijoto 38 “centigrade”
  • Kuumwa na kichwa, kujihisi uchovu wa mwili na maumivu ya misuli
  • kutokwa na makamasi mepesi yanayotiririka bila ukomo na kuwashwa na koo.

Madhara ya ugonjwa wa mafua ya ndege ni pamoja na:

  • Kupata shida wakati wa kupumua (Acute Respiratory Distress)
  • Kushindwa kufanya kazi kwa viungo mbalimbali vya mwili (multi-organs failure)
  • Homa ya mapafu na
  • Maambukizi katika damu (septicemia)

Ili kulinda afya za wananchi na jamii ya Zanzibar kwa ujumla, ZFDA inapenda kuwataarifu kwamba inasitisha kutoa vibali vya uingizaji wa bidhaa za ndege “poultry meat & poultry products” kutoka nchini UKRAINE na POLAND  kuanzia leo Jumatano tarehe 29 mwezi Januari mwaka 2020 hadi pale usalama wa bidhaa hizo utakapothibitishwa na mamlaka husika.

Sambamba na zuio hilo, ZFDA inawaomba wananchi na jamii ya Zanzibar kutoa taarifa juu ya uwepo wa bidhaa zinazotoka nchi hizo katika soko la Zanzibar kuanzia kipindi kilichotokea mripuko wa maradhi hayo. Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA), inaendelea kufanya kazi zake ikiwemo ukaguzi ili kugundua uwepo wa bidhaa zote za chakula zisizokidhi viwango ili kuweza kuilinda jamii na maambukizi ya madhara yatokananyo na bidhaa zisizo salama.

ZFDA inawashauri wananchi na jamii yote ya Zanzibar kuondokana na mazoea ya matumizi ya bidhaa za vyakula ambazo hazijapitia taratibu za uingizaji nchini, pia kuepuka kula nyama ya ndege(kuku, bata, njiwa) mbichi au isiyoiva vizuri hali inayoweza kupelekea kupata maambukizi kupitia vimelea ili kupunguza uwezekano wa maambukizi, kuepuka kuhifadhi vyakula kwa kuvichanganya vile vilivyokuwa tayari kwa kula na ambavyo havijapikwa ili kuepuka kuambukiza chakula kilichokua tayari kuliwa.

Kwa  wasafiri, ni muhimu kuepuka kutembelea maeneo wanapouzwa au kufungwa ndege hususani sehemu zilizoripotiwa au kuhisiwa kuwa na miripuko ya ugonjwa huu. Pia inasisitizwa kujenga na kuendeleza tabia ya kukosha mikono kwa maji safi na salama kabla na baada ya kula.

Ahsanteni.

Imetolewa na;

Mkurugenzi Mtendaji,

Wakala wa Chakula na Dawa,

S.L.P 3595,

Mombasa – Zanzibar.

Simu:+255 24 233 3959/ +255 778 705 626,+255 (0) 777 139 968

barua pepe: info@zfda.go.tz

Please follow and like us: