ZANZIBAR FOOD AND DRUG AGENCY

Together We Protect Public Health

cropped-ZFDA.jpg

UWEPO WA TAARIFA INAYOSAMBAA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII KUHUSU DAWA YA CARBOTOUX YENYE KUSABABISHA MADHARA KWA MTUMIAJI

Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA), inapenda kutoa taarifa kwa umma kuhusu video inayosambaa katika mitandao ya kijamii kuanzia tarehe 26/11/2023, ikimuonesha mtu anaetapika damu huku ikihusishwa na utuamiaji wa Dawa aina ya CARBOCISTEINE-PROMETHAZINE SYRUP yenye jina la biashara la CARBOTOUX” iliyotengenezwa na kampuni ya PHARMA PRODUCT MANUFACTURING ya nchini CAMBODIA. Mzungumzaji katika audio yenye taarifa hiyo alieleza kuwa tukio hilo limetokea nchini Msumbiji na Dawa hiyo inapatikana katika nchi za Msumbiji na nchi jirani ikiwemo Afrika Kusini na Tanzania.

ZFDA inapenda kuutaarifu umma kwamba ina mifumo madhubuti ya kuhakikisha Dawa zote zinazoingia Zanzibar zinafata utaratibu uliowekwa ili kuhakikisha kuwa ni salama na zenye ubora na ufanisi unaotakiwa. Ikiwa lengo kuu ni kuhakisha afya za wananchi wa Zanzibar zinalindwa na kuimarishwa wakati wa utumiaji wa Dawa.

Hivyo, ZFDA inapenda kuuhakikishia umma kwamba Dawa hiyo ya CARBOTOUX inayosambaa kupitia video katika mitandao ya kijamii, haipo katika soko la Zanzibar na wala haijasajiliwa kwa ajili ya kutumiwa hapa Zanzibar. Aidha Dawa zote zinazopata ruhusa ya kuingizwa Zanzibar zinafata taratibu za usajili ikiwemo vifungashio vyake kuwa na lugha ya Kiswahili au Kiingereza au zote.

Mwisho, ZFDA inapenda kuwaomba wananchi kuripoti madhara ambayo yanasababishwa na utumiaji wa Dawa au uwepo wa bidhaa ambazo ubora, usalama na ufanisi wake wanautilia mashaka ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa manufaa ya umma.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA HABARI,

WAKALA WA CHAKULA NA DAWA, ZANZIBAR.

27/11/2023

Kwa maelezo zaidi fika ofisi zetu zilizopo Mombasa, Unguja na Wete, Pemba au wasiliana nasi kupitia anuani zifuatazo:

S.L.P 3595, Mombasa, Changu, Zanzibar, Simu: + 255 24 2233959-, Nukushi: +255 24 2233959, Tovuti: www.zfda.go.tz, Barua pepe: info@zfda.go.tz