TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA KWA UMMA

KUONDOA ZUIO LA UINGIZAJI WA BIDHAA ZA NYAMA KUTOKA  AFRIKA KUSINI

Mnamo tarehe 8 Machi 2018 Wakala wa chakula, Dawa na Vipodozi –ZFDA ilizuia rasmi uingizaji wa bidhaa za nyama kutoka Afrika Kusini kutokana na kutangazwa kwa mripuko  mkubwa wa maradhi ya Listeria (Listeriosis Outbreak) nchini humo.

Ugonjwa huu wa Listeria unasababishwa na vimelea vya bakteria aina ya Listeria monocytogenes ambao hupatikana katika udongo, maji na mboga mboga. Bidhaa za chakula zitokanazo na wanyama na mboga mboga zipo katika hatari zaidi ya kubeba vimelea hivi. Wanyama na binadamu hupata maambukizi ya ugonjwa huu kutoka katika vyanzo hivi vyenye vimelea vya Listeria.

Kutokana kutangazwa kwa upungufu wa matukio ya ugonjwa huo na Idara ya Afya nchini humo (South Africa Department of Health) ZFDA inaondoa zuio hilo kuanzia leo tarehe 31.10.2018 kwa kuweka tahadhari zifuatazo:

Waingizaji wote wa bidhaa tajwa hapo juu wataendelea kufuata taratibu zote za uingizaji wa bidhaa za Chakula ikiwemo kufanyiwa ukaguzi wa kiwanda (GMP Inspection) kinachozalisha bidhaa hizo kabla ya kuanza taratibu za uingizaji.

ZFDA inawashauri wananchi na jamii yote ya Zanzibar kuondokana na mazoea  ya kutumia  vyakula bila kuvipika ipasavyo, hali inayoweza kupelekea kupata maambukizi kupitia vimelea vilivyo hai, kuepuka kuhifadhi vyakula kwa kuchanganya vile vilivyokua tayari kwa kula na ambavyo havijapikwa ili kuepuka kuambukiza chakula kilichokua tayari kuliwa.  Pia inasisitizwa kujenga na kuendeleza tabia ya kuosha mikono kwa maji safi na salama kabla na baada ya kula

 

Ahsanteni.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mtendaji

Wakala Wa chakula,Dawa na Vipodozi Zanzibar

Kwa taarifa Zaidi wasiliana na:

Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) kupitia barua pepe

info@zfda.go.tz

Pakua tangazo hili hapa….

UZINDUZI WA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA ZFDA (ZFDA E-PORTAL) 29 MACHI 2018

UZINDUZI WA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA ZFDA (ZFDA E-PORTAL) 29 MACHI 2018

Mfumo wa kielektroniki umezinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Bibi HARUSI SAID SULEIMAN akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Hamad Rashid Hamad siku ya Tarehe 29 Machi 2018 katika ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar Resort Kibweni. Mfumo huu utaleta mageuzi ya mfumo uliozoeleka wa karatasi na kuwepesisha wadau wa ZFDA kupata urahisi wa huduma kwa njia ya mtandao. Mafanikio hayo yamefikiwa chini ya msaada mkubwa wa TradeMark East Africa (TMEA) ndani ya Program maalum ya “East Africa Community Medicine Regulatory Harmonization” (EAC-MRH read more about MRH programme…).

Mfumo huo upo teyari kutumika na tunaendelea kutoa maelekezo ya utumiaji wa mfumo ndani ya afisi zetu zilokuepo Mombasa Zanzibar.

 

TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA YA KUTOKEA KWA MRIPUKO WA LISTERIA NCHINI AFRIKA KUSINI

Mripuko wa ugonjwa wa listeria (listeriosis) ulioripotiwa kujitokeza nchini Afrika  Kusini tangu mwezi wa Januari mwaka 2018 kama ni mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa listeria kutokea katika kumbukumbu za Shirika la Afya Duniani (World Health Organization – WHO)

Katika taarifa ya Waziri wa Afya nchini Afrika Kusini juu ya hali ya mripuko wa Listeria iliyotolewa mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka 2018, inataja kuthibitishwa jumla ya kesi kutoka watu 948 zimeripotiwa ambapo watu 659 wamethibitishwa kupata maambukizi na watu 180 kati ya walioambukizwa wameshapoteza maisha.

Ugonjwa huu wa Listeria unasababishwa na vimelea vya bakteria aina ya Listeria monocytogenes ambao hupatikana katika udongo, maji na mbogamboga. Bidhaa za chakula zitokanazo na wanyama na mbogamboga zipo katika hatari zaidi ya kubeba vimelea hivi. Wanyama na binadamu hupata maambukizi ya ugonjwa huu kutoka katika vyanzo hivi vyenye vimelea vya Listeria.

Ugonjwa wa Listeria huwa na dalili zifuatazo kutegemea na hali ya aliyeambukizwa:

  • Mafua, homa, kuharisha, kutapika, mwili kukosa nguvu na maumivu ya mwili
  • Septisemia (maambukizi kwenye damu)
  • Maambukizi kwenye ubongo (meningitis)

Mama mjamzito yupo katika hatari kubwa ya kupoteza ujauzito kutokana na ugonjwa wa Listeria. Watoto wadogo, wazee na watu wenye magonjwa yanayodhoofisha mfumo wa kinga ya mwili (mf. HIV, kansa, kisukari, magonjwa ya ini na figo ya muda mrefu n.k)

Ili kulinda afya za wananchi na jamii ya Zanzibar kwa ujumla, Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar inasitisha kutoa vibali vya uingizaji wa bidhaa za nyama aina ya polony na sausages zenye majina ya Viennas, Frunkfurturs, Russians, Bokkie, Renown, lifestyle na Meliekip ambazo hutoka katika makampuni ya Enterprise Food Production na Rainbow Chicken Limited yote ya Afrika Kusini, kuanzia leo Alkhamis tarehe 8 mwezi Machi mwaka 2018 hadi pale usalama wa bidhaa hizo utakapothibitishwa na Wizara ya Afya ya Afrika Kusini.

Sambamba na zuio hilo, ZFDA inawaomba wananchi na jamii ya Zanzibar kutoa taarifa juu ya uwepo wa bidhaa hizo katika soko la Zanzibar. Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA), inaendelea kufanya kazi zake za ukaguzi na uchunguzi  ili kugundua uwepo wa bidhaa za chakula zilizotajwa zinazotoka Afrika Kusini pamoja na bidhaa zote za chakula zilizo katika hatari ya kupata maambukizi ya vimelea vya bakteria wanaosababisha Listeria.

ZFDA inawashauri wananchi na jamii yote ya Zanzibar kuondokana na mazoea ya matumizi ya bidhaa za vyakula ambazo hazijapitia taratibu za uingizaji nchini, pia matumizi ya vyakula bila kuvipika, hali inayoweza kupata maambukizi kupitia vimelea vilivyo hai, kuepuka kuhifadhi vyakula kwa kuvichanganya vile vilivyokuwa tayari kwa kula na ambavyo havijapikwa ili kuepuka kuambukiza chakula kilichokua tayari kuliwa.  Pia inasisitizwa kujenga na kuendeleza tabia ya kukosha mikono kwa maji safi na salama kabla na baada ya kula

 

Ahsanteni.

Kwa taarifa Zaidi wasiliana na:

Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) kupitia barua pepe

info@zfda.go.tz

au piga simu: +255 (0) 777 139 968

S.L.P 3595 Barabara ya Changu, Mombasa,

ZANZIBAR, TANZANIA

KUPITIA MIONGOZO YA ZFDA KWA WADAU WA CHAKULA

KUPITIA MIONGOZO YA ZFDA KWA WADAU WA CHAKULA

KUPITIA MIONGOZO YA ZFDA KWA WADAU WA CHAKULA

Katika kuboresha kazi zake ZFDA imepitia miongozo yake ya chakula ili kuweza kufikia matarajio ya wateja wake. Ushirikishwaji wa wadau ni jambo muhimu sana kwetu katika kuifahamu na kuifanyia kazi miongozo hiyo, ili kuiwezesha taasisi kufikia malengo iliyojiwekea.

Tunaomba wadau wetu kushiriki kikamilifu kwa kutumia muda wao kupitia miongozo iliyokuwepo hapo chini na kutupatia mapendekezo na maoni ili tuweze kuiboresha.

 

Maoni yataendelea kupokelewa mpaka tarehe 25 Novemba 2017 kupitia njia zifuatazo:

Tovuti: www.zfda.go.tz

Baruapepe: info@zfda.go.tz

Simu: +255 777139968

Kuwasilisha moja kwa moja katika ofisi zetu zilizopo Mombasa (Barabara ya Changu), Zanzibar.

Limetolewa na;

Mkuu wa Kitengo cha Idara ya Udhibiti wa Chakula

Dr. KHAMIS ALI OMARSTAKEHOLDERS FOOD GUIDELINES REVIEW

ZFDA reviewed its food guidelines for the service improvements to meet customers’ satisfaction. Stakeholders’ engagement is most important for the successful understanding and implementation of those guidelines.

We kindly ask our dear customers and public in general to review the guidelines attached hereunder and give their valuable advice and comments so as to improve them.

 

The comments will be received until 25th November 2017 through the following:

Website: www.zfda.go.tz

E-mail: info@zfda.go.tz

Mobile phone: +255 777139968

Directly submission at ZFDA Head Office , Mombasa (Changu Road), Zanzibar.

Issued by:

HEAD OF FOOD SAFETY CONTROL DEPARTMENT

Dr. KHAMIS ALI OMAR


 

UFAFANUZI KUHUSU UWEPO WA MCHELE WA PLASTIKI.

UFAFANUZI KUHUSU UWEPO WA MCHELE WA PLASTIKI.

ZFDB ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya – Zanzibar inayosimamia udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa na vipodozi, moja kati ya kazi zake ni kuhakikisha kuwa bidhaa hizo ni salama kabla kufika kwa watumiaji.
Hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko kutoka wa watu mbalimbali juu ya uwepo wa mchele unaosadikiwa kuwa ni wa plastiki na madhara yake kiafya. Malalamiko hayo yameanza katika mitandao ya kijamii na kuendelea kufikishwa kwetu kwa njia nyengine mbali mbali za mawasiliano, baada ya kupokea malalamiko hayo na pia kuzingatia hali inayoendelea hivi sasa, ZFDB inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao.
Ukaguzi uliofanywa na unaoendelea kufanywa na wakaguzi wa ZFDB haujagundua wala kubaini uwepo wa mchele wa aina hio katika soko la Zanzibar. Vile vile hakuna uthibitisho wowote uliopatikana juu ya uwepo wa mchele huo pamoja na madhara yake kiafya.
Aidha, kuna vipande vidogo vidogo vya video vinavyosambaa katika mitandao ya kijamii ambavyo hutoa upotoshaji kwa watumiaji wa bidhaa hio na wananchi kwa ujumla. Hoja zinazosambazwa kupitia mitandao hio zimekijkita katika kudunda kwa mchele uliopikwa baada ya kufinyangwa. Ukweli ni kwamba kudunda huko kwa mchele baada ya kupikwa na kufinyangwa ni moja ya tabia za asili za mchele (natural properties of rice) zinazosababishwa na uwepo wa virutubisho vya aina ya amylose na amylopectin. Uwiano wa virutubisho hivi unatofautiana baina ya aina za mchele, kadiri uwiano huu unavyoongezeka ndipo tabia hii ya asili ya kudunda pia huongezeka. Kwahio ipo michele ambayo ina kiwango kikubwa cha uwiano huo na ipo pia yenye kiwango kidogo, hivyo basi kudunda dunda kwa mchele haina maana kuwa ni plastiki kwa vile michele yote inao uwezo huo wa kudunda.
ZFDB inapenda kuwatoa khofu na wasiwasi watumiaji wa bidhaa za mchele pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kuwa bidhaa hio ni salama kutumika na hakuna tatizo la plastiki lililogundulikana wala kuthibitishwa hadi sasa. ZFDB inaomba ushirikiano kwa wananchi katika kutoa taarifa zozote kwa afisi yake endapo kutakuwa na haja ya kupata ufumbuzi zaidi.

 

Imetolewa na Afisi ya Mrajis
ZFDB
14.07.2017

Maangamiza Zaidi ya Tani 62 za Bidhaa Zilizoharibika

Maangamiza Zaidi ya Tani 62 za Bidhaa Zilizoharibika

Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar Yaangamiza Zaidi ya Tani 62 za Bidhaa Zilizoharibika kwa Matumizi ya Binaadamu.
30.11.2016
Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDB) imeangamiza zaidi ya tani 62 za vyakula vibovu na vilivyopitwa na wakati katika zoezi lililofanyika Kibele Mkoa Kusini Unguja.
Mkuu wa Idara ya Biashara na Uendeshaji wa ZFDB Ndugu Abdulaziz Shaib Mohd amesema bidhaa hizo mbovu zinatokana na tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kujenga matumaini ya kuingiza faida kwa bidhaa wanazouza bila kuangalia usalama wa bidhaa hizo kwa afya za watumiaji.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi la kuangamiza bidhaa hizo, Ndugu Abdulaziz ambae pia ni Mkuu wa operesheni wa uangamizaji amesema bidhaa hizo zimegundulika kufuatia operesheni iliyofanywa na Bodi katika maghala na maduka mbali mbali ya Unguja.
Amesema ZFDB ambayo moja ya jukumu lake ni kusimamia ubora na usalama wa chakula, dawa na vipodozi kwa matumizi ya wananchi, itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maghala yanayowekwa bidhaa na kwenye maduka ili kuhakikisha jukumu hilo linafanikiwa.
Amewataka wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa wananchi wenzao na kujuwa kwamba biashara mbovu ama zilizopitwa na wakati ni sumu na zinaweza kudhofisha afya zao.
Mkuu wa Idara ya Chakula wa ZFDB bibi Aisha Suleiman amesema mchango mkubwa wa raia wema ndio uliofanikisha kugundulika bidhaa mbovu na zilizopitwa na wakati katika maduka na maghala mbali mbali.
Hata hivyo amewataka wananchi kujenga tabia ya kuchunguza tarehe ya kumaliza muda bidhaa wanazonunua na wanapogundua bidhaa imepitwa na wakati watoe taarifa katika Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Wakati huo huo Afisa Mkuu wa Idara ya Dawa na Vipodozi wa ZFDB Ndugu Mwadini Ahmada Mwadini amesema vipodozi haramu vilivyokamatwa baadhi yake vinakemikali zenye sumu na hazifai kwa afya ya binadamu.
Amewashauri wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha biashara ya dawa na vipodozi kushirikiana na Bodi hiyo kwa lengo la kulinda afya za wananchi.
Dawa zilizoangamizwa katika operesheni hiyo ni mafuta ya kula lita 10,105, sukari tani 2.15, mchele tani 26, tende tani 10, bidhaa mchanganyiko za mboga mboga tani 13, dawa na vipodozi tania tatu.

disposal-3 disposal-2 disposal-1 disposal-6 disposal-5