WAKALA WA CHAKULA NA DAWA KUYAFUNGIA MACHINJIO YASIO NA VIWANGO

WAKALA WA CHAKULA NA DAWA KUYAFUNGIA MACHINJIO YASIO NA VIWANGO


Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeahidi kusimamia na kudhibiti ubora wa machinjio ya ng’ombe na yatakayobainika hayana kiwango cha kufanya kazi hiyo yatafungiwa ili kuhakikisha wananchi wanapata chakula kilicho salama kwa afya zao.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Dkt. Khamis Ali Omar ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea machinjio ya Kinyasini,Donge Muwanda na Mahonda katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kuangali mazingira na ubora wa machinjio hayo.

Amesema juhudi za Serikali kupitia Wakala wa Chakula na Dawa ni kuhakikisha wananchi wanapata chakula kilichoandaliwa katika ubora unaostahiki ambao utamlinda mtumiaji asipatwe na madhara.

Alisema Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar walianzisha kanuni ya kuwataka wananchi wanaosafirisha nyama ya ngombe kwa ajili ya biashara kutumia gari maalum za kusafirisha kutoka machinjioni kwa lengo la kulinda usalama wa chakula hicho

Dkt. Khamis amezitaka taasisi zinazosimamia suala la uingizaji wa ngombe ikiwemo Idara ya Mifugo, na Kilimo Wakaguzi pamoja na vyombo vya ulinzi kuwa na mashirikiano ya pamoja ili kuhakikisha ngombe hawachinjwi katika mazingira hatarishi.

Diwani wa Wadi ya Mahonda Haji Fadhil Mkadam amewaomba Wakala wa Chakula na Dawa kuwasaidia kumaliza ujenzi wa chinjio lao liweze kuanza kazi ili kuepuka usumbufu na kuvunja sheria ya kuchinja ngombe katika sehemu zisizorasmi.

Wakala wa Chakula na dawa wanaendelea kulizuwiya Chinjio la Mahonda lisifanye kazi kutokana na kukosa mahitaji maalum yanayotakiwa kuwepo kabla ya kuanza kazi za kuchinja ng’ombe.

Akizungumza na wakaguzi wa wakala wa chakula na dawa Mmiliki wa Chinjio la Kinyasini Abdalla Mohamed amesema wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuhakikisha sehemu yake ya kazi iko katika mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli hizo.

Aliwashukuru wakaguzi wa chakula kufanya ziara za mara kwa mara kwa lengo la kuwapa maelekezo ya kuweka mazingira safi katika sehemu za machinjio.

Awali Mkaguzi wa Chakula Maulid Khamis Shaabani wa chinjio la Kinyasini alisema wamekuwa wakifanyakazi usiku na mchana kufuatilia usalama wa ng’ombe wanaofikishwa katika sehemu hiyo kwa ajili ya kuchinjwa na wakigundua kasoro wanazuia kazi isiendelee.