UFAFANUZI KUHUSU UWEPO WA MCHELE WA PLASTIKI.

UFAFANUZI KUHUSU UWEPO WA MCHELE WA PLASTIKI.

ZFDB ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya – Zanzibar inayosimamia udhibiti wa bidhaa za chakula, dawa na vipodozi, moja kati ya kazi zake ni kuhakikisha kuwa bidhaa hizo ni salama kabla kufika kwa watumiaji.
Hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko kutoka wa watu mbalimbali juu ya uwepo wa mchele unaosadikiwa kuwa ni wa plastiki na madhara yake kiafya. Malalamiko hayo yameanza katika mitandao ya kijamii na kuendelea kufikishwa kwetu kwa njia nyengine mbali mbali za mawasiliano, baada ya kupokea malalamiko hayo na pia kuzingatia hali inayoendelea hivi sasa, ZFDB inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao.
Ukaguzi uliofanywa na unaoendelea kufanywa na wakaguzi wa ZFDB haujagundua wala kubaini uwepo wa mchele wa aina hio katika soko la Zanzibar. Vile vile hakuna uthibitisho wowote uliopatikana juu ya uwepo wa mchele huo pamoja na madhara yake kiafya.
Aidha, kuna vipande vidogo vidogo vya video vinavyosambaa katika mitandao ya kijamii ambavyo hutoa upotoshaji kwa watumiaji wa bidhaa hio na wananchi kwa ujumla. Hoja zinazosambazwa kupitia mitandao hio zimekijkita katika kudunda kwa mchele uliopikwa baada ya kufinyangwa. Ukweli ni kwamba kudunda huko kwa mchele baada ya kupikwa na kufinyangwa ni moja ya tabia za asili za mchele (natural properties of rice) zinazosababishwa na uwepo wa virutubisho vya aina ya amylose na amylopectin. Uwiano wa virutubisho hivi unatofautiana baina ya aina za mchele, kadiri uwiano huu unavyoongezeka ndipo tabia hii ya asili ya kudunda pia huongezeka. Kwahio ipo michele ambayo ina kiwango kikubwa cha uwiano huo na ipo pia yenye kiwango kidogo, hivyo basi kudunda dunda kwa mchele haina maana kuwa ni plastiki kwa vile michele yote inao uwezo huo wa kudunda.
ZFDB inapenda kuwatoa khofu na wasiwasi watumiaji wa bidhaa za mchele pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kuwa bidhaa hio ni salama kutumika na hakuna tatizo la plastiki lililogundulikana wala kuthibitishwa hadi sasa. ZFDB inaomba ushirikiano kwa wananchi katika kutoa taarifa zozote kwa afisi yake endapo kutakuwa na haja ya kupata ufumbuzi zaidi.

 

Imetolewa na Afisi ya Mrajis
ZFDB
14.07.2017